26 Mei 2024 - 18:36
Takwa la Bunge la Kiarabu la kusimamishwa mara moja mauaji ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza

Katika kikao kilichofanyika katika makao makuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Cairo, Spika wa Bunge la Kiarabu ametaka kusitishwa mara moja jinai na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Akizungumza jana Jumamosi katika makao makuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu huko Cairo, mji mkuu wa Misri, Spika Adel al-Asoumi ametaka kusimamishwa mara moja jinai na mauaji ya umati yanayoendelea kufanywa kwa miezi minane sasa na utawala haramu unaoukalia kwa mabavu Quds Tukufu, huko Gaza.

Katika kikao hicho, kutokana na kuendelea mauaji ya kimbari ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ripoti ya Kamati ya Palestina ilichunguzwa kwa kina, ambapo waliohudhuria kikao hicho wametaka kusitishwa mara moja vita vya mauaji hayo ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na hatua madhubuti kuchukuliwa na jamii ya kimataifa kwa ajili ya kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni katika ukanda huo. Katika taarifa yake siku ya Ijumaa, Bunge la Kiarabu limelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kuulazimisha utawala ghasibu wa Kizayuni utekeleze uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kusimamisha mara moja mashambulizi yake dhidi ya Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza. Baada ya kupita takriban miezi minane tangu utawala ghasibu wa Kizayuni uliposhambulia Ukanda wa Gaza, utawala huo haujafanikiwa lolote katika malengo yake zaidi ya kufanya mauaji ya kimbari, uharibifu, jinai za kivita, ukiukaji wa sheria za kimataifa, kushambulia mashirika ya misaada ya kibinadamu na kusababisha njaa dhidi ya watu wa Gaza. Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde za Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, tangu kuanza kwa mashambulizi ya utawala huo wa kigaidi katika ukanda huo tarehe 7, Oktoba 2023, mwaka jana Wapalestina elfu 35,903 wameuawa shahidi na wengine elfu 80,420 wamejeruhiwa.

342/